Tuesday, October 8, 2013

Wadau 520 wakutana kuzungumzia huduma bora za uzazi wa mpango

WATAFITI na wadau wa huduma za uzazi za mpango 520 watakutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango kufahamishana juu ya matokeo ya tafiti yaliyofanyika nchini.

Mkutano huo utafunguliwa na Rais Jakaya Kikwete, atazindua nyota ya kijani ya uzazi wa mpango yenye ujumbe; “Fuata Nyota Ya Kijani, Upate Mafanikio” utaongozwa na dhima; “kupata ufumbuzi wa changamoto tulizo nazo ili kusukuma mbele jitihada za kuboresha huduma za uzazi wa mpango”.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema mkutano huo utatoa fursa ya kufahamishana matokeo ya tafiti zilizofanyika, kubadilishana uzoefu kuhusu mambo yanayohusu uzazi wa mpango na kukubaliana mipango ya kuendeleza na kuboresha huduma hizo.

Mkutano huo wa kitaifa utahudhuriwa na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi, utawawezesha washiriki kukubaliana jinsi ya kuboresha huduma zake kwa kutilia maanani changamoto zilizopo, uzoefu uliopatikana na fursa zilizopo ili kupata njia zenye kufaa zaidi katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango nchini.

Mkutano pia utatoa fursa kwa wadau wa uzazi wa mpango nchini kuweka maazimio yatakayosaidia katika kuinua kiwango cha uzazi wa mpango kufikia lengo la Taifa la asilimia 60 ya watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango ifikapo mwaka 2015.

“Wawakilishi toka ngazi mbalimbali za Serikali kuanzia ngazi ya taifa, mikoa na wilaya wawakilishi toka asasi za kiraia, wadau wa maendeleo na sekta ya watu binafsi wataweka maazimio yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma za uzazi wa mpango kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 27 na kufikia lengo la Taifa la asilimia 60 ya watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango ifikapo 2015,” imesema taarifa hiyo.

Mkutano huo wa kitaifa ni matokeo ya mkutano wa Kimataifa wa Uzazi wa Mpango uliofanyika jijini London, nchini Uingereza Julai, mwaka jana, uliotoa changamoto kwa dunia kuhusu umuhimu wa kuongeza kiwango cha watumiaji wa huduma ya uzazi wa mpango kwa hiari katika nchi 69 zinazoendelea. 

Katika mkutano wa London, nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, wadau wa asasi za kiraia kutoka duniani kote ziliazimia kuongeza jitihada ili kufikia lengo la kimataifa la kuwafikia akina mama na wasichana 120 milioni wenye mahitaji ya huduma za uzazi wa mpango ifikikapo mwaka 2020.


0 comments:

Post a Comment